Mastaa wa Bongo Waliouaga Ukapera Mwaka Huu

MAISHA ya mastaa ulimwenguni mwote yamejaa anasa na starehe kwa sana. Mawazo ya kuoa au kuolewa hayapewi nafasi kubwa vichwani mwa wengi.
masanja798
Hata hivyo kwa mastaa wa mbele, imekuwa kawaida kwao kuoana ndoa za mikataba, kisha kusitisha katika muda waliopanga. Lakini siku za karibuni, mambo yamekuwa tofauti ambapo mastaa wengi wameamua kuoana kwa ndoa za kidini.
Hapa Bongo kwa vile hakuna utaratibu wa ndoa za mikataba, kwa muda mrefu suala la ndoa kwa mastaa limekuwa halipo sana miongoni mwao, bali kuwa kwenye uhusiano wenyewe kwa wenyewe na kumwagana baada ya muda.
Baadhi ambao walibahatika kuingia kwenye ndoa, hawakudumu. Baada ya vipindi fulani walimwagana na kila mtu akaendelea na maisha yake.
Yote kwa yote, listi ya mastaa wanaoingia kwenye ndoa siyo kubwa ukilinganisha na wingi wao na kuwa na umri sahihi unaowaruhusu kuingia kwenye ndoa.
Miaka ya karibuni tumeshuhudia ndoa za mastaa mbalimbali wakiwemo Irene Uwoya, Mrisho Zimbwe ‘Tito’, William Mtitu, Jimmy Mafufu, Rashid Makupa ‘Kupa’, Paul James ‘PJ’ na wengineo.
Lakini mwaka huu kasi ya mastaa walioingia kwenye ndoa ni kubwa kulinganisha na miaka mingine, jambo linaloashiria kuwa wameamua kuachana na maisha ya anasa na kuingia kwenye ndoa kama inavyoelekezwa na vitabu vitakatifu.
Hapa chini, Juma3tata inakudondoshea listi ya mastaa wa mbalimbali ambao kwa mwaka huu wameingia kwenye ndoa.
Inawezekana idadi ni zaidi ya hii lakini hapa tunakueletea wale maarufu zaidi ambao wapo kwenye makabrasha yetu.
WASTARA
Mwigizaji mwenye hisia kali, Wastara Juma ndiye staa wa kwanza kufungua dimba la kuingia kwenye ndoa mapema mwezi Januari, mwaka huu.
Wastara alifunga ndoa na Mbunge wa Jimbo la Donge mjini Zanzibar, Sadifa Khamis Juma,  ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM).
Hata hivyo, ndoa hiyo haikudumu kwani miezi mitatu tu baadaye iliota mbawa.
MR BLUE
Aprili mwaka huu, mkongwe wa Bongo Fleva, Heri Samir ‘Mr Blue’ alitoa mkono wa kwaheri kwa klabu ya makapera baada ya kufunga ndoa na mpenzi wake wa siku nyingi Waheeda, ambaye ni mzazi mwenzake.
Uamuzi wa Mr Blue kuachana na ukapera umeendeleza imani kuwa muziki wa Bongo Fleva siyo uhuni hasa kwa sababu mwanamke aliyemuoa ni mzazi mwenzake kama ilivyo kwa FA.
NDOA YA MR blue-1
NANCY SUMARI
Miss World Africa 2005 akitokea Miss Tanzania mwaka huo, Nancy Sumari Juni, mwaka huu aliamua kuachana na ukapera na kuoana na Luca Neghesti.
Ndoa yao ilifuatiwa na sherehe ya kukata na shoka iliyofanyika jijini Arusha. Nancy ni miongoni mwa warembo wachache kutoka Miss Tanzania ambao wamejipa heshima kwa kuamua kuingia kwenye ndoa.
Wengi wanaendelea kuishi maisha ya kula bata, wakisahau kuwa umri unakwenda.
MWANA FA
Staa wa Bongo Fleva ambaye alitamba vilivyo na wimbo wake wa Bado Nipo Nipo, Hamisi Mwinjuma ‘Mwana FA’ naye hakukubali mwaka huu uishe kabla hajaingia kwenye ndoa.
Alifunga ndoa hiyo mwezi Juni, mwaka huu na mpenzi wake wa siku nyingi Helga ambaye amezaa naye mtoto mmoja kabla ya ndoa hiyo.
Baadhi ya mastaa waliohudhuria ndoa yake hiyo ni pamoja na  Ambwene Yesaya ‘AY’, Hermy B, Ommy Dimpoz, Sallam, Dully Sykes, Alberto Msando na wengine wengi.
MWANAFA23
SHAMSA FORD
Diva katika kwianda cha filamu za Kibongo, Shamsa Ford naye anaongeza idadi ya mastaa walioamua kuachana na ukapera.
Ndoa ya Shamsa ilifungwa wiki iliyopita, Sinza, jijini Dar es Salaam na mumewe Chid Mapenzi, katika uhusiano unaelezwa kuwa ni wa muda mfupi lakini uliozaa ndoa.
shamsa33
FINA MANGO
Agosti, mwaka huu ilikuwa zamu ya mtangazaji noma Bongo, Fina Mango ambaye aliolewa na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya KVTC, Hans Lemm.
Fina ni miongoni mwa waasisi wa Kipindi cha Power Breakfast cha Clouds FM, kabla ya kuondoka na kujiunga na Magic FM ambapo alikuwa akitangaza Kipindi cha Makutano.
Ndoa ya wawili hawa ilifungwa na sherehe yao  kufanyikia jijini Arusha.
GERALD HANDO
Mtangazaji wa Kipindi cha Joto la Asubuhi, Radio E FM, Gerald Hando naye ameingia kwenye listi hii baada ya kufunga ndoa na Miriam Kitenge.
Hando alifunga ndoa hiyo mwezi Agosti, mwaka huu ambapo hafla ilichukua nafasi katika Ukumbi wa Golden Tulip, Posta jijini Dar es Salaam.
Kabla ya kujiunga na E FM yeye na maswahiba wake Paul James ‘PJ’ na Abel Onesmo, walikuwa Radio Clouds FM.
MASANJA
Komediani anayetisha kwa utajiri Bongo, Emmanuel Mgaya ndoa yake na mrembo aitwaye Monica  bado haijapoa kwani naye walifunga ndoa hiyo mwezi uliopita.
Ndoa hiyo ilifungwa katika Kanisa la Mito ya Baraka lililopo Kariakoo jijini Dar es Salaam na Mchungaji Bruno Mwakiborwa aliyehudumu katika ibada hiyo.
Kutokana na ustaa wake, ndoa yake ilikuwa na vivutio vingi ikiwemo vimbwanga vya mshereheshaji, rafiki yake Mc Pilipili ambaye ni komediani maarufu kama alivyo Masanja.
Mbali na hilo, watu wengi maarufu walihudhuria wakiwemo viongozi wa serikali wakiwemo Naibu Spika wa Bunge la Tanzania Dk. Tulia Ackson,  mawaziri, wabunge na viongozi wengine.
Mbali na Naibu Spika, Dk. Tulia viongozi wengine waliohudhuria ni Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Dk. Charles Tizeba na wabunge Willium Ngeleja (Sengerema) na Hussein Bashe (Nzega Mjini).

No comments: