Header Ads

Okwi, Bocco waipaisha Simba

Ushindi wa Simba umeifanya timu hiyo kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu msimu huu bali pia umeongeza pengo la pointi baina yake na Yanga wanaoshika nafasi ya pili kufikia nane.
Matokeo hayo ya leo yameifanya Simba ifikishe pointi 55 katika michezo 23 ambayo imeshacheza kwenye Ligi Kuu hadi sasa wakati Yanga iliyocheza jumla ya mechi 22, yenyewe ina pointi 47.
Okwi na Bocco ambao wamekuwa na kiwango bora cha kufumania nyavu msimu huu, walionyesha mapema jinsi walivyopania kuutumia mchezo huo kuzidi kujiimarisha kwenye chati ya ufungaji bora msimu huu kutokana na jinsi walivyokuwa wakiwaweka mabeki wa Mbeya City kwenye wakati mgumu.
Kasi ya nyota hao wawili iliisaidia kwa kiasi kikubwa Simba kumaliza mchezo ndani ya dakika 45 za kwanza tu za mechi hiyo ambayo ilionekana ni ya upande mmoja kutokana na Mbeya City kuelemewa.
Kwa kulidhihirisha hilo, Okwi aliifungia Simba bao la kuongoza dakika ya 16 tu ya mchezo baada ya kufanya kazi nzuri ya kumalizia mpira uliopanguliwa na kipa Owen Chaima wa Mbeya City kufuatia shuti la John Bocco.
Kabla ya hapo Okwi na Bocco walipoteza nafasi takribani tatu nzuri ambazo iwapo wangekuwa makini, zingeifanya Simba imalize kipindi cha kwanza ikiwa na idadi kubwa ya mabao.
Kuingia kwa bao hilo ni kama kuliiongezea makali zaidi Simba ambayo iliendelea kupeleka mashambulizi langoni mwa Mbeya City ambayo yalizaa matunda kwa kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 33 lililofungwa na Asante Kwasi aliyemalizia kwa kichwa krosi ya Kichuya.
Mbeya City walionekana kutoridhishwa na uamuzi wa refa Hans Mabena kukubali bao hilo wakidai kwamba mfungaji alikuwa ameotea na kutokana na kumzonga mwamuzi huyo, kipa wake Chaima alijikuta akionyeshwa kadi ya njano.
Hata hivyo, dakika mbili baadaye Frank Ikobela aliipatia Mbeya City bao la kwanza baada ya kuunganisha vyema kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na Majaliwa Shaban.
Furaha ya Mbeya City kwa bao hilo ilidumu kwa sekunde kadhaa tu kwani Simba ilipata bao la tatu ndani ya dakika hiyohiyo kupitia kwa John Bocco ambaye aliunganisha kwa ustadi pasi ya Shomari Kapombe.
Kutokana na safu ya kiungo ya Mbeya City kuonekana kupwaya, kocha wake Ramadhan Nsanzurwimo alilazimika kumfanyia mabadiliko Babuu Ally na nafasi yake kumuingiza Hamidu Mohammed hata hivyo mabadiliko hayo yakuwasaidi

No comments: